Katika kitabu cha 'Starved for Science, How Biotechnology is being kept out of Africa' cha Mwandishi Robert Paarlberg kuna hoja nyingi juu ya kwanini wakulima wengi barani Afrika ni maskini kutokana na kupuuza teknolojia za uzalishaji katika secta ya kilimo.
Katika nchi yetu, wakulima wetu na jamii imepotoshwa kuhusu
ukweli halisi wa uhandisi Jeni au Genetically Modified Organism. Hii
inatokana na wananchi wengi kusikiliza hoja za upande mmoja ambazo
hazina uthibitisho wa kitafiti wala kisayansi kuhusu faida za teknolojia
hii. Inawezekana zipo sababu nyingi zinazosababisha hali hii zikiwemo
uelewa mdogo wa wananchi kuhusu maana hasa ya teknolojia hii na
uthibitisho wa kitafiti na kisayansi kuhusiana na ukweli wa teknolojia
hii.Wananchi wasipoelimishwa maana na umuhimu wa teknolojia hii,
inawezekana kabisa nchi yetu ikachelewa sana kufanya mapinduzi ya
viwanda kupitia Tafiti,Sayansi na Teknolojia katika kilimo chetu.
Kwa
muda sasa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia
majukwaa mbalimbali yakiwemo Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya
Kilimo Tanzania(OFAB) pamoja na wadau mbalimbali wa kilimo imekuwa
ikifanya jitihada kuelimisha wananchi kuhusiana na faida za kutumia
teknolojia ya uhandisi Jeni. COSTECH inafanya hivi kwakuwa imepewa
mamlaka na Sheria No 7 ya Bunge ya Mwaka 1986 kuratibu na kuendeleza
tafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu.
Pamoja
na jitihada hizi za COSTECH na wadau wengine wa kilimo, changamoto
inaonekana ni kubwa sana hususani kwa baadhi ya vikundi kupotosha maana
halisi ya teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO) kwamba teknolojia hii ina
madhara kwa afya ya Binadamu.
Mtafiti
anayeheshimika sana Duniani katika masuala ya utafiti na magonjwa ya
Kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Mikocheni Dr Joseph
Nduguru anabainisha kuwa teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO) ni teknolojia
ambayo ina lengo la kuongeza mavuno kwa mkulima. Anaeleza kuwa
kinachofanyika katika teknolojia hiyo ni kutengeneza kinga kwa mmea au
mfugo au ili usipate Mashambulizi ya magonjwa.
"Kinachofanyika
kwenye teknolojia ya uhandisi Jeni hakina tofauti sana na teknolojia
inayotumika wakati wa kutengeneza dawa ya Insulini kwa ajili ya wagonjwa
wa Kisukari"analeza Dr Ndunguru.
Dr Ndunguru anatoa mfano wa ugonjwa wa mihogo ujulikanao kama Bato Bato ambao ameufanyia utafiti kwa kipindi kirefu. Anasema ugonjwa huo unasababishwa na aina fulani ya Kirusi aitwaye cassava mosaic virus ambaye
huyafikia majani ya muhogo kupitia inzi wadogo weupe. Akizungumzia
jinsi teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO) inavyofanyika kwenye mihogo, Dr
Ndunguru anasema kuwa kinachofanyika ni kuchukua mbegu ya muhogo na
kuipandikizia aina ile ile ya kirusi ambayo huuathiri muhogo. Baada ya
mchakato huo muhogo uliopandikiziwa ile DNA ya kile kirusi huwa na kinga
na haiwezi tena kushambuliwa na aina ile ya Kirusi. Kwa maneno mengine
muhogo ule uliofanyiwa uhandisi Jeni huwa imara kukabilina na aina ile
ya ugonjwa wa Bato bato.
Teknolojia
ya uhandisi Jeni ambayo imefanyiwa majaribio mengi katika Taasisi ya
Kilimo ya Mikocheni ikihusisha wataalamu wengi kutoka mataifa makubwa
Duniani imethibitisha kuwa mimea yote inayotokana na teknolojia hii
haina madhara kwa Binadamu.
Juma
Shaaban ambaye ni Mkulima wa mihogo huko Bagamoyo, Shamba lake
limeathiriwa vibaya na aina hiyo ya virusi lakini hafahamu kama mihogo
yake ina ugonjwa. Yeye anaamini tu kwamba majani ya mihogo yake
yamekauka kutokana na ukame na ndiyo maana hupata mavuno kidogo ya
mihogo.
Shina
la Muhogo ulioathiriwa na virusi vya ugonjwa huo likikatwa na kupandwa
sehemu nyingine bado hali ya ugonjwa huendelea kuwepo na kuambukiza eneo
hilo pia.
Dr Ndunguru anaendelea kueleza kuwa virusi vinavyosababisha magonjwa ya mimea kama muhogo (cassava mosaic virus) havina madhara kwa binadamu na ndiyo maana kisamvu cha muhogo ulioathiriwa na ugonjwa wa bato bato huliwa na watu wengi bila kufahamu.
Professor
Calistius Juma kutoka Chuo Kikuu cha Harvard Marekani, naye katika
tafiti zake mbali mbali anaeleza kuwa teknolojia ya Uhandisi Jeni haina
madhara kwa Afya ya Binadamu. Anaeleza kuwa nchi kama Afrika Kusini,
Burkinafaso, Misri na Sudan zinatumia Teknolojia hii na kumekuwepo na
ongezeko kubwa katika mazao.
Wakati
nazungumza na mwanazuoni huyo, nilibaini kuwa nchi yetu imeweka
utaratibu mzuri, tunaweza kabisa kutumia Uhandisi Jeni kwenye kilimo
hususan maeneo ambayo hayana rutuba. Nchi ya India ni mfano wa mataifa
ambayo yanazalisha pamba kwa wingi Duniani kuliko Tanzania pamoja na
kuwa ardhi yao haina rutuba ya kutosha kama tuliyo nayo.
Watu
wamekuwa wakijiuliza; kwanini teknolojia hii inapigwa vita sana na
baadhi ya watu na Taasisi? Jibu ni rahisi tu, mbegu za mazao ambazo
zimefanyiwa uhandisi Jeni zina kinga ambayo hustahimili magonjwa hivyo
mkulima anaweza asitumie kabisa mbolea. Kwa maneno mengine, kama
tukiruhusu sheria zetu zikubali moja kwa moja Uhandisi Jeni, kuna baadhi
ya viwanda vitakosa soko na biashara ya baadhi ya mbolea inaweza
kuharibika.
Katika
baadhi ya mihadhara ambayo COSTECH ilikaribisha wataalamu kuelezea
faida za Uhandisi Jeni, zimekuwa zikiibuliwa hoja ambazo hazina msingi
wala ushahidi wa kisayansi. Baadhi ya watu wamekuwa wakipotosha umma
kuwa mazao yatokanayo na uhandisi Jeni yana madhara kwa binadamu na ni
mkakati wa nchi za magharibi kufanya biashara.
Hoja
hizi ambazo hazina mashiko ya kitafiti wala kisayansi hazina msingi kwa
kuwa hutolewa kutokana na sababu za kibiashara za kuhofia teknolojia
hii inaweza kuua soko la viwanda vya pembejeo. Uhandisi Jeni ni
teknolojia nzuri ambayo kama tutaitumia vizuri bila kukubali propaganda
za baadhi ya vikundi vya watu vyenye matakwa yao ya kibiashara, inaweza
kuharakisha zaidi maendeleo ya kilimo chetu na hatimaye kutusaidia
katika mapinduzi makubwa ya viwanda na uchumi wa nchi yetu.
Teknolojia
hii imekwishafanyiwa tafiti za kutosha na wataalamu wetu nchini
wakiwemo wale wa Taasisi ya Kilimo ya Mikocheni. Tunaweza kabisa kufanya
Uhandisi Jeni tukiwa hapa hapa nchini tena kwa kuhusisha mbegu zetu
hizi hizi tulizo nazo. Uhandisi Jeni hauna maana ya kuchanganya mbegu
mbili zenye asili tofauti na kuziweka pamoja ili kupata mbegu chotara.
Uhandisi Jeni ni hali ya kupandikiza DNA ya kirusi cha ugonjwa flani
unaoathiri mmea katika mmea husika ili kujenga kinga kwa mmea huo.
Mwandishi wa Makala hii ni Afisa Uhusiano Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
No comments:
Post a Comment